#subscribe on youtube "YOHANEC CHANG'A"
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Parokia ya Buhingo, Jimbo Kuu la Mwanza
Tukio hili hufanyika siku ya Alhamisi Kuu wakati wa Misa ya Karamu ya Bwana. Tukio hili hufanywa ili kukumbuka tukio la Yesu kuwaosha miguu wanafunzi wake wakati wa Karamu ya Mwisho. Kutokana na Israeli kuwa nchi yenye joto kali mara nyingi miguu iliwaka moto na kutoa jasho jingi lililosababisha miguu kutoa harufu mbaya.
Tendo la Yesu kuwaosha miguu wanafunzi wake lilikuwa na maana kubwa tatu:
(i) Kuonesha roho ya utumishi. Kwa tendo hili Yesu anafundisha kuwa kiongozi/mkubwa kwa hadhi anapaswa kujishusha na kuwatumikia wale anaowaongoza. Viongozi hawapaswi kubaki juu kama matawi ya miti bali wanapaswa kushuka chini kama mizizi ya miti na kuwatumikia watu. Wazazi kadhalika wanapaswa kujibidiisha kutumikia familia zao.
(ii) kuonesha roho ya unyenyekevu. Ni tendo la unyenyekevu mkubwa sana bwana kujishusha na kuosha miguu ya watumwa/watumishi wake. Kazi ya kuosha miguu ilikuwa ni kazi duni sana kuliko zote miongoni wa Wayahudi. Hivyo kwa tendo hili Kristo anajinyenyekesha na kuonekana kama mtumwa ambaye anaosha miguu. Hata Maandiko Matakatifu yanadokeza hali hii ya Kristo kujifanya mtumwa inatuonesha kuwa sisi nasi tunapaswa kujishusha katika maisha na hata kutimiza kazi zile ambazo zinatazamwa kuwa kazi duni. Tusiwe watu wa kujikweza na wenye majivuno bali wanyenyekevu kwa mfano wa Kristo mwenyewe.
(iii) dokezo juu ya Sakramenti ya Upatanisho. Tendo la Yesu kuwaosha miguu wanafunzi wake ni kiashiria cha umuhimu wa Sakramenti ya Kitubio. Kukataa kwa makusudi Kristo atuoshe uovu/dhambi zetu kunatufanya tusiwe na ushirika naye: dhambi zetu zinatufanya tusiwe na ushirika na Kristo. Kadhalika, Yesu ametupa jukumu la kutawadhana sisi kwa sisi: Hivyo, kwa nafasi ya kwanza Mapadre wanapaswa kuwatawadha waamini wao kwa sakramenti ya Kitubio na Upatanisho na kwa nafasi ya pili, sisi sote tunapaswa kutawadhana maovu yetu sisi kwa sisi kwa njia ya kuonyana kidugu, kwa njia ya kukemea uovu na kwa njia ya kuombeana wongofu. Tusiwe kwa kwanza kuhukumu.
Uwe na maandalizi mema ya Pasaka.
Comments
Post a Comment