#subscribe on youtube "YOHANEC CHANG'A"
Fahamu maana ya tukio la Altare kubaki tupu (misalaba, vitambaa na mapambo kuondolewa Altareni)
Tukio hili hufanyika mara tu baada ya adhimisho la Misa ya Karamu ya Bwana siku ya Alhamisi Kuu. Mara baada ya Misa hii Altare huvuliwa- misalaba, vitambaa na mapambo yote huondolewa altareni na hivyo Altare hubaki wazi kabisa.
Kwa nini Altare hubaki tupu au wazi? Altare humwakilisha Kristo, hivyo kitendo cha Altare kuvuliwa vitambaa na mapambo mengine (yaani Altare kubaki tupu) hutukumbusha tukio la Yesu kuvuliwa nguzo zake na kubaki mtupu baada ya kukamatwa: “Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, “Salamu, Mfalme wa Wayahudi!” (Mt. 27:28-29). Pia pale msalabani Yesu alivuliwa nguo zake (rejea Yn. 19:23; rejea pia Kituo cha 10 cha Njia ya Msalaba). Kadhalika, kitendo cha vitambaa na mapambo kuondolewa Altareni kinaashiria tendo la uhai wa Kristo kuondolewa kwa ajili ya wokovu wetu. Kadhalika, tendo la kuondoa misalaba, vitambaa na mapambo altareni linaashiria kukoma kwa Adhimisho la Misa hadi itakapofanyika Misa ya Kesha la Pasaka.
Uwe na maandalizi mema ya Ijumaa Kuu na hatimaye Pasaka.
Comments
Post a Comment