Hayati Dkt John Pombe Magufuli enzi za uhai wake.
na yohanec chang'a TV
NIANZE na kipi? Mtetemo wa sauti ya Mama Samia Suluhu Hassan akitangaza kifo chake au mshtuko wa watanzania baada ya kusikia hatunaye tena? Au nianze na wingi wa marais na viongozi wa nje walioshiriki mazishi yake?
Labda nianze na umati wa watanzania waliojitokeza kila kituo alichopitishwa kwa ajili ya kuagwa, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza au Zanzibar? Sielewi nianze na kipi.
Pengine nianze na idadi ya watu waliopoteza maisha yao kutokana na msiba wake. Mapenzi yao kwake ndio yaliyosababisha wapoteze maisha yao. Inasisimua kwa kweli.
Ni nani huyu ninaemzungumzia? Mwanamajumui na Mwanamapinduzi halisi wa Afrika, Kiongozi mwenye haiba ya uongozi, Jiwe, Mcha Mungu na Jasiri halisi.
Namzungumzia mtoto aliyezaliwa kwenye tumbo la Mama wa Kiafrika pale Chato, Geita Tanzania. Mtoto wa Mzee Joseph na Mama Suzan. Mseminari aliyeyatoa maisha yake kwa ajili ya watanzania.
Jina lake ni Dk John Magufuli. Rais wa mioyo ya watanzania ambaye sasa amelala kwenye kaburi lake nyumbani kwake Chato. Sehemu aliyoipenda na kuwa na wivu nayo haswa.
Hatutomuona tena kwa sasa, hatutoisikia tena sauti yake. Kwake umekua usiku tayari na sina budi kumtakia Usiku Mwema.
Ni nani haswa huyu Dk John Magufuli? Ni nani haswa hata apendwe na watanzania kwa kiwango kikubwa namna hii? Sijapata kuona mazishi yaliyojaa idadi kubwa ya watu na yenye kufuatiliwa kama yake.
Kwa umri wangu huu uliozidi robo karne nimeshuhudia mazishi ya Papa John Paul, nimeona mazishi ya Gwiji wa Muziki wa Pop duniani, Michael Jackson.
Achana na huko duniani, hapa nyumbani nimeshuhudia mazishi ya viongozi wakubwa serikalini, viongozi wakubwa kiroho, wasanii na watu mashuhuri lakini mazishi ya Dk John Magufuli yamejawa na simulizi nyingi zisizoisha.
Wingi wa watanzania kila ambapo mwili wa Dk Magufuli ulipitishwa kwa ajili ya kuagwa ulitosha kuyaonesha mapenzi yao kwake.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa alikua na msemo wake unasema, "Tanzania imeona, Afrika imeona na Dunia nzima imeona".
Hakika kila mmoja ameshuhudia namna Dk Magufuli alivyozikwa kwa upendo wa hali ya juu. Hata waliomchukia na kumbeza salam zimewafikia.
Ni kwanini azikwe kwa upendo mkubwa na wingi wa watu kiasi kile?
Tazama. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa idadi ya watu waliofuatilia mazishi ya Dk Magufuli akiagwa kitaifa jijini Dodoma duniani kote ni Bilioni 3.9 karibu watu Bilioni nne. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) takwimu za mwaka 2020 zinaonesha idadi ya watu duniani kote ni Bilioni 7.9.
Hii ni kusema kuwa nusu ya watu duniani kote ilifuatilia mazishi ya mpendwa wetu Jumatatu iliyopita Machi 22 jijini Dodoma.
Hii ina maana Dk Magufuli amevunja rekodi ya wingi wa watu waliofuatilia mazishi ya aliyekua Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni, Papa John Paul wa II aliyefariki April 2005.
Samahani kwa kuchepuka. Turejee njia kuu.
Idadi hiyo kubwa ya watu inaonesha jinsi gani watu walivyoguswa na msiba wake, kifo chake kiliishtua Dunia. Uwezo wake wa uongozi na namna alivyolikabili janga zito la ugonjwa wa Corona ni sababu iliyochangia mabilioni ya watu kufuatilia mazishi yake.
Je nifunge safari hadi Chato nikamtafute Dk Magufuli kaburini kwake alipolala? Hapana. Nifanyeje basi?
Njia ni moja na rahisi tu, nitaenda kumtafuta mioyoni mwa watanzania ambao kwa miaka takribani sita alifanya kazi ya kushiriki changamoto zao, kuzitatua na kuwaletea maendeleo..
' He turned us from doubters to believers' yaani ndie binadamu aliyetufanya tuamini na kuondoa mashaka mioyoni mwetu. Alituambia atapambana na mafisadi na kweli akapambana nao.
Alituahidi 2015 kuwa Tanzania itafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, matokeo yake tukafikia uchumi wa kati mwaka 2020 miaka mitano kabla ya mwaka ululiokusudiwa. Kasi ya namna gani hii?
Alituahidi biashara ya dawa za kulevya itakoma Tanzania na kweli ikakoma, wale wazungu wa unga walipaona Tanzania pachungu tu kwa sababu ya umwamba wa Dk Magufuli katika misimamo yake ya kuwaepusha watanzania na athari ya dawa za kulevya.
Walipomwita Dikteta yeye alijenga Reli ya Umeme itakayokua inapitisha Treni ya Mwendokasi ambayo kipande cha Dar hadi Morogoro kimekamilika tayari huku kile cha Morogoro hadi Makutupora kikiwa jirani kukamilika.
Maguberi yalipotangaza propaganda chafu dhidi yake Dk Magufuli alijenga vituo 500 vya afya Nchi nzima ndani ya miaka mitano. Vingi kuliko nyakati zote za Nchi yetu.
Sauti hii ivuke milima na mabonde iwaeleze wale walafi kuwa Dk Magufuli ambaye amelala kaburini ndiye aliyerudisha nidhamu serikalini, watumishi wa serikali wakawaona wananchi ndio Maboss zao na kuwaheshimu.
Umati uliojitokeza kumuaga Dk Magufuli ni ishara isiyo na kificho kwamba amegoma kufa na anaishi mioyoni mwa watanzania. Wanaozusha na kumsema waseme wanavyotaka lakini jina lake tumelichora kwa muhuri wa moto mioyoni mwetu.
Stendi ya Kisasa pale Mbezi Louis, Stendi ya Kisasa Dodoma, 'Fly Over' ya Ubungo, mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere kule Rufiji, wingi wa mapato yetu kwa mwezi zaidi ya Trilioni moja, vituo vya afya, ndipo ambapo sisi tutaenda kumtafuta Dk Magufuli wetu..
Angalia watu walivyokua wakilia pale uwanja wa Uhuru, tazama mapokezi yake Dodoma tena usiku, hebu kaangalie wingi wa watu kule Zanzibar.
Halafu uone watu walivyokua wakilifuata gari lililobeba mwili wake kule Mwanza, walipita nae kila mahali hakuna aliyetamani kumuona Dk Magufuli akiondoka, tulimpenda na daima hatutomsahau.
Nitaimiss sauti yake kali yenye mamlaka, nitakumbuka roho yake yenye huruma na 'Ukristo' ndani yake, sitosahau alivyowapenda waislamu licha ya kwamba haikua imani yake.
Tutammiss Jiwe haswa, Jasiri asiyeitishwa wala kuogopa yoyote.
Ukitaka kujua maana ya Rais jasiri rejea namna alivyowashughulikia wale jamaa wa Barick na Accasia.
Machozi tuliyotoa kwa ajili yake, wingi wa watu waliojitokeza kumuaga yote hiyo ilikua kwa ajili ya Rais wao. Rais wa mioyo yao, binadamu aliyetuelewa na sisi tukamuelewa.
Bado mtaandika kwamba alikua Dikteta? Aibu yenu Maguberi na Walafi wa Madaraka maana kama ni hivyo basi watanzania wote sisi ni madikteta.
Kama ilivyokua kwa Mwalimu Nyerere, Thomas Sankara, Kwame Nkurumah, Abraham Lincoln na Martin Luther King au Patrice Lumumba ndivyo itakavyokua kwa John Magufuli hajafa hatokufa tutaendelea kuishi nae kila tutakapokumbuka alivyohamishia makao makuu ya nchi Dodoma.
Tutaendelea kuishi nae kila tutakapoiona Stiglers Gorge, kila tutakapoona Ndege zetu alizonunua kwa fedha zetu wenyewe. Tutaishi nae kila tutakapokumbuka alivyoimudu Corona.
KWAKO MAMA SAMIA
Sina mengi kwako kwa leo maana najua bado una machungu ya kuondokewa na kiongozi na mtu aliyekuamini sana.
Lakini wewe ni Mama na nikukumbushe kuwa watoto wengi waliolelewa na Mama bila Baba walifanikiwa sana maishani mwao. Baba ameondoka, umebaki Mama yetu tunaamini tutafanikiwa tukiwa na wewe. Tunajua unatupenda na sisi tunakupenda.
Nitarudi kwako siku nyingine, kwa sasa wacha nimtakie Dk John Magufuli Usiku Mwema.
Comments
Post a Comment